Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtalaam huru Tom Nyanduga aeleza wasiwasi wake juu ya haki za binadamu Somalia

UN Photo/Tobin Jones)
Wakimbizi wa ndani nchini Somalia. Picha ya

Mtalaam huru Tom Nyanduga aeleza wasiwasi wake juu ya haki za binadamu Somalia

Mjini Geneva, mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu ukiendelea, mtalaam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia, Bahame Tom Nyanduga, amelielezea baraza hilo wasiwasi wake kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Somalia.

Amesema, miongo miwili ya vita, vitishio vya ugaidi na udhaifu wa mamlaka za serikali zimeathiri haki za binadamu nchini humo, hasa kwa wanawake, wazee na watoto. Kwa jumla amesema, hali ya kibinadamu katika maeneo yaliyotawaliwa na kundi la Al-shabab ni ya kutia wasiwasi zaidi.

Aidha, akiongea na redio ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, amepongeza juhudi zilizofanyika na mamlaka za kimataifa pamoja na serikali ya Somalia ili kurejesha hali ya utulivu na kukomboa eneo la Kati Kusini, akisikitishwa na kuona kwamba haki za raia wa kawaida na waandishi wa habari zinatishiwa wakati huu wa vita dhidi ya ugaidi. Ametoa mifano ya kufungwa kwa wanadishi wa habari na kusimamishwa kwa redio.

Halikadhalika Tom Nyanduga ameelezea wasiwasi wake juu ya ripoti za ukatili wa kijinsia kutoka jeshi la Somalia na la Ujumbe wa Muungano wa Afrika, AMISOM, akiomba hatua zichukuliwe ili kupeleka wahanga wa ukatili huo mbele ya sheria.

Hata hivyo, akiongea na Redio ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, amekaribisha juhudi za serikali katika kujenga mamlaka bora na kuandaa katiba mpya, akitumai kuwa utaratibu huo utakamilika ifikapo mwaka 2016 jinsi ulivyopangwa.

(Sauti ya Nyanduga)

Hatimaye ameonya kuwa vita vinavyoendelea nchini humo vimesababisha ukosefu mkubwa wa chakula na hivyo kutaka juhudi zaidi zifanyike ili kunusuru usalama wa chakula kwa raia wa Somalia.