Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjadala Mkuu wa Kikao cha 69 cha Baraza Kuu waanza rasmi

UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu Ban Ki-moon(kushoto),Sam Kahamba Kutesa (kati kati) na Tegegnework Gettu.

Mjadala Mkuu wa Kikao cha 69 cha Baraza Kuu waanza rasmi

Mjadala Mkuu wa Kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, umeanza rasmi leo, kwenye ukumbi wa Baraza hilo uliopewa sura mpya. Taarifa kamili na Abdullahi Boru.

(Taarifa ya Abdullahi)

Ni Katibu Mkuu Ban Ki-moon, akitangaza kufunguliwa rasmi kwa ukumbi wa Baraza Kuu, ambao umekarabatiwa na kupewa sura mpya.

Muda mfupi baadaye, Ban amelihutubia Baraza Kuu, akitoa ripoti yake iliyogusia mambo mseto, akilaani ugaidi na siasa inayogawanya watu na vitendo vya kibaguzi. Ban amezungumzia pia juhudi za kutokomeza umaskini na kufikia maendeleo endelevu, akisisitiza maendeleo haya yanapaswa kuwa jumuishi

Mabadiliko ndilo lengo letu. Siwezi kufikiria mahali bora pa kuanzia kuliko kufungua milango na kuondoa vizuizi kwa wanawake na wasichana. Hatuwezi kutimiza asilimia 100 ya uwezo wa ulimwengu kwa kuwaacha nje asilimia 50 ya watu duniani. Kuchukua hatua kuhusu tabianchi ni nguzo ya matumaini yetu yote”

Katika hotuba yake, Rais wa Baraza Kuu Sam Kutesa, amesema hatua zimepigwa kufikia malengo ya milenia, lakini bado kuna kazi nyingi ya kufanya

Takriban watu bilioni moja bado wamenaswa katika umaskini uliokithiri. Kwa hiyo, ni lazima tutoe kipaumbele kwa kutokomeza umaskini katika ajenda yetu mpya ya maendeleo. Kuhusu afya, ni lazima tuongeze juhudi za kukabiliana na HIV na Ukimwi, malaria na kifua kikuu. La msingi wakati huu ni kukomesha kusambaa kwa Ebola na kuwapa matibabu waathiriwa.”