Nchi za Asia-Pasifiki imarisheni soko la ndani badala ya kutegemea soko la nje pekee: Ripoti

24 Septemba 2014

Wakati ukanda wa Asia Pasifiki umesalia kuwa eneo lenye chagizo kubwa ya uchumi wa dunia, biashara na uwekezaji, ripoti mpya inaonyesha kuwa bado mwelekeo huo haujarejea kama ulivyokuwa kabla ya mdororo wa uchumi duniani.

Ripoti hiyo kuhusu biashara na uwekezaji Asia Pasifiki mwaka 2014 iliyochapishwa na Tume ya Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Asia na Pasifiki, ESCAP imeonyesha kuwa jumla ya biashara ya uingizaji na uuzaji bidhaa nje kwa mwaka 2013 iliongezeka kwa asilimia Mbili tu huku ikidhoofika katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.

Katibu Mtendaji wa ESCAP Dkt. Shamshad Akhtar amesema ripoti hiyo licha ya kuonyesha matarajio ya ukuaji wa uchumi huo kwa asilimia Saba mwakani, bado kuna mambo yanayotia shaka kwa kuangalia vigezo vya uchumi mkubwa wa dunia.

Kwa mantiki hiyo amekariri ripoti hiyo ikitaka kuweka mizania ya shughuli za kiuchumi ikiwemo kujikita zaidi katika kuongeza thamani ya bidhaa za nchi zinazouzwa nje.

Halikadhalika ripoti imetaka kubadili mwelekeo wa kujikita zaidi katika kuuza bidhaa nje ya nchi ikiwemo Marekani na Ulaya na badala yake kuimarisha soko la ndani na kwenye ukanda huo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter