Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi ni wajibu wa mwanadamu- Museveni

UN Photo/Amanda Voisard
Yoweri Museveni, rais wa Uganda,

Mabadiliko ya tabianchi ni wajibu wa mwanadamu- Museveni

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi ni wajibu wa mwanadamu. Akizungumza wakati wa mkutano wa tabianchi Jumanne Septemba 23, Rais Museveni amesema kuwa mienendo ya maisha katika nchi fulani yanatia uhai wa mwanadamu hatarini.

“Nimeghadhibishwa mno na upungufu wa barafu vileleni mwa milima Ruwenzori na Kilimanjaro. Kupoteza kwa barafu vileleni mwa milima Ruwenzori na Kilimanjaro, kwa sababu ya kuongezeka joto, ambako kumesababishwa na wengine, ni uvamizi mbaya kwa urithi wa watu wa eneo la tropikali la Afrika, na pia uvamizi kwa kazi ya ajabu ya Mungu. Kuwepo theluji kwenye Ikweta ulikuwa kweli ni muujiza, ambao sasa umo hatarini.”

Rais Museveni amesema kinachosikitisha ni kwamba, uharibifu huu haufanywi na Afrika, bali ni uharibifu unaotekelezwa na Amerika ya Kaskazini, Ulaya na maeneo fulani ya Bara Asia.

“Hii ni aina mpya ya uvamizi dhidi ya bara la Afrika na watu wake ambao siku zote wanatendewa ubaya.”

Museveni amesema kuwa kuendeleza huduma za umeme Afrika na kulinda misitu ya Kongo na maeneo ya unyevuunyevu ni njia mwafaka ya kulinda mazingira, na kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Baada ya hotuba ya Rais Museveni, Waziri wa Mambo ya Maji na Mazingira, Daktari wa Ephraim Kamuntu amezungumza na Redio ya Umoja wa Mataifa, na kueleza wanachokitaka:

“Hatutafuti kosa. Tunataka tu nchi zilizoendelea kutambua kwamba mabadiliko ya tabianchi yanatuathiri vilevile hata kama tunachangia kiasi kidogo. Kwa hiyo nchi zenye uwezo bora, teknolojia na pesa zaidi, zinapaswa kufanya vile vile kama njia ya usawa ili kusaidia nchi zinazoendelea ili tuwe pamoja, kwa sababu tumeathirika pamoja.”