Haki ya mazingira safi iwe haki ya binadamu: Jan Eliasson
Wakati mkutano wa dunia kuhusu mabadiliko ya tabianchi ukiendelea mjini New York leo Jumanne tarehe 23 Septemba, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, ambaye ameongoza mojawapo ya vikao vya viongozi kwenye mkutano huo, amesema haki ya mazingira inapaswa kuwa haki ya binadamu.
Akizungumza na idhaa hii, Jan Eliasson amesema hatua zinahitajika kwa ngazi ya kitaifa ili kukabiliana na suala hili ambalo linaigusa dunia nzima.
Ameongeza kwamba, nchi zilizokumbwa na vita bado haziwezi kuweka swala la mazingira kwenye ajenda yao, tukipaswa kukumbuka kwamba hakuna amani bila maendeleo wala maendeleo bila amani na heshima ya haki za binadamu, akisema haki ya mazingira inapaswa kuwekwa kipaumbele kama haki ya binadamu.
Aidha amesema mkutano huo wa leo umewakumbusha viongozi wa dunia kuhusu umuhimu wa kujali mambo yenye matokeo ya muda mrefu:
“ Kama kuna kitu nilichojifunza katika miaka hii yote, ni kwamba tunapaswa kuzuia, si tu kwa ajili ya kuzuia mizozo bali pia kusikiliza dalili kutoka mazingira. Tunapaswa kuishi kwa amani na mazingira yetu. Nimepatanisha mizozo mingi. Ningependa sasa kupatanisha amani na mazingira. Lakini ni vigumu kupata yule atakayekaa kwenye meza ya mazungumzo. Kwa hiyo sisi nchi wanachama na mashirika yasiyo ya kiserikali tunapaswa kuwakilisha upande huu ambao ni kimya, yaani mazingira”