Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali na Sekta ya kibinafsi Kushirikiana katika kupunguza kwa nusu Umaskini wa Nishati

Katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, Kenya. Picha ya UNHCR - Kenya

Serikali na Sekta ya kibinafsi Kushirikiana katika kupunguza kwa nusu Umaskini wa Nishati

Siku moja kabla ya Mkutano wa viongozi kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, mchakato wa Ushirikiano wa Nishati Endelevu kwa Wote umetoa ahadi mpya ya kuchochea uwekezaji kwa kutoa nafasi ya upatikanaji huduma ya nishati endelevu kwa mamia ya watu.

Ushirikiano kati ya mkakati wa Nishati Endelevu kwa Wote, Muungano wa Ulaya na Mpango wa Marekani wa nishati Afrika- US Power Africa, unaolenga kupunguza umaskini wa nishati kwa nusu kwa watu bilioni 1.3 walio "maskini wa nishati” duniani ni hatua muhimu katika kufikia azimio la upatikanaji wa nishati kwa wote kufikia mwaka wa 2030 kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa.

Kufikia sasa, watu bilioni 1.3, au karibu mtu mmoja kati ya watu watano duniani hawana umeme. Wakati huo huo, idadi maradufu ya watu hawa- yaani watu bilioni 2.6- bado wanategemea kuni, mkaa, au taka itokanayo na mazao au aina nyingine za nishati kupika chakula chao na kupasha joto nyumba zao.

Tathmini ya Benki ya Merrill Lynch, Benki ya Kitaifa ya Maendeleo ya Brazil na Benki ya Dunia inathibitisha uwezekano kwa kutoa mpango halisi wa kuongeza dola bilioni 120 katika uwekezaji ambao utachangia kupunguza umaskini na kuendeleza suluhu la upatikanaji wa nishati endelevu.

Kandeh Yumkella, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Nishati Endelevu, amesema kuna vyombo sita ambavyo vimevumbuliwa mathalan, upanuzi wa vyombo vya hati thamani ya fedha, kutoka kiwango cha sasa cha dola bilioni 23 kwa mwaka, hadi dola bilioni 50 au dola bilioni 60 kwa mwaka.