Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awaomba Marais wa ukanda wa maziwa makuu waungane ili kupambana na FDLR

Ray Virgilio Torres, mkuu wa ofisi ya MONUSCO kwenye mkoa wa Kivu Kaskazini, akihesabu silaha zinazorudisha na kundi la FDLR. Picha ya MONUSCO.

Ban awaomba Marais wa ukanda wa maziwa makuu waungane ili kupambana na FDLR

Viongozi wa Ukanda wa Maziwa Makuu, Jumatatu ya tarehe 22 septemba wamejadili kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, mkutano wa nne wa mpango wa amani, usalama na ushirikiano kwa ajili ya DRC ukifanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Katika uzinduzi wa mkutano huo wa Nne uliohudhuriwa na viongozi wa ukanda huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amekaribisha juhudi zilizofanyika katika kupambana na wanamgambo wanaoathiri usalama wa mashariki mwa DRC, akisema hali ya usalama imeimarika.

Hata hivyo, amesema, changamoto bado zipo ikiwemo hali ya kutoaminiana baina baadhi ya nchi ya ukanda huo huku akisisitiza umuhimu wa kusitisha shughuli za kundi la waasi wa FDLR.

(sauti ya Ban)

Nawaomba kuendeleza mpango mzima wa kukabiliana na FDLR kupitia nyenzo zisizo za kijeshi, na ikiwa lazima kupitia hatua za kijeshi. Tunapaswa kutumia nguvu zote ili kutokomeza hali ya ukosefu wa utulivu inayoathiri mamilioni ya watu na inayoathiri pia maendeleo na ukuaji wa uchumi katika ukanda huo kwa muda mrefu mno”

Ameziomba nchi zote za Ukanda wa maziwa makuu na jamii ya kimataifa kuendelea kuzungumza na sauti moja huku akisema ni muhimu kujenga hali ya uaminifu baina nchi zote za ukanda huu.

Halikadhalika, ameongeza kuwa chaguzi zinatarajiwa kufanyika katika nchi mbalimbali za ukanda huo kwa kipindi cha miaka michache ijayo, akisema anatumaini zitakuwa fursa za kuimarisha demokrasia kwenye ukanda huo.