Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasiwasi kuhusu mafua ya ndege wazuka tena Asia; kuku, bata bukini hatarini:FAO

Kuku hawa wakifanyiwa ukaguzi na mamlaka ya afya nchini Thailand.(Picha ya FAO)

Wasiwasi kuhusu mafua ya ndege wazuka tena Asia; kuku, bata bukini hatarini:FAO

Shirika la Chakula na Kilimo FAO limetangaza kuhusu mlipuko mpya wa mafua ya ndege aina ya AH5N6 huko eneo la kusini mashariki mwa Asia, likisema ni tishio kubwa kwa afya ya mifugo na uchumi.

Visa vya kwanza vimeripotiwa China mwezi wa April mwaka huu, na hivi karibuni visa vingine vimegunduliwa huko Laos na Vietnam.

Afisa Mkuu wa Utabibu wa Wanyama wa Fao, Juna Luborth, amesema virusi vya mafua vinaendelea kubadilika na kuwa vitisho vipya;

"Kwa sababu tunaona H5N6 katika nchi tatu tofauti Asia mashariki na magharibi ambako imeenea sana , lakini kwa sababu tunajua kwamba virusi vya homa hubadilika na kusambaa sana tunapaswa kuwa makini tutayarishe maabara, huku wahudumu wa afya wakifanya ukaguzi unaohitajika kuona kama kuna mabadiliko katika kirusi hiki ama uwepo wa kirusi kingine."

FAO imesema ugonjwa huo unaoathiri kuku na bata bukini ni tishio kwa uchumi wa mamilioni ya watu wanaotegemea ndege hao kama njia ya kujipatia kipato barani Asia.

Halikadhalika, Mtalaam huyo wa FAO amesema hakuna hatari kubwa ya maambukizi kwa binadamu ambapo hadi sasa ni mtu mmoja tu aliyeripotiwa kuambukizwa.

WHO na FAO wanaendelea kushirikiana na serikali za nchi husika ili kufuatilia hali ya mlipuko huo na kuhakikisha hatua zinazohitajika zinachukuliwa.