Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaongeza misaada kwa wakimbizi wa Syria wanaoongezeka Uturuki, yasifu Uturuki

Picha ya © UNHCR/L.Addario

UNHCR yaongeza misaada kwa wakimbizi wa Syria wanaoongezeka Uturuki, yasifu Uturuki

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNCHR limeongeza huduma zake za utoaji misaada ili kuisaidia serikali ya Uturuki kuwasaidia wakimbizi wa Syria wapatao 70,000 ambao wameingia nchini Uturuki katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Mamlaka za serikali ya Uturuki zinajiandaa kwa uwezekano wa mamia ya maelfu ya wakimbizi kuwasili katika siku zijazo, wakati wapiganaji wanapoung’ang’ania mji wa Koban au Ayn al-Arab kaskazini mwa Syria na kuwalazimu watu zaidi kukimbia makwao.

Kamishna Mkuu wa UNHCR, António Guterres amepongeza ukarimu wa Uturuki wa kuwakaribisha na kuwasaidia wakimbizi hao ambao ghafla wamelazimishwa kutoroka makwao kwa sababu ya machafuko. Ameongeza kuwa idadi hiyo kubwa ya wakimbizi wanaoingia Uturuki inaonyesha umuhimu wa kuwapa hifadhi wakimbizi wa Syria, na pia haja ya kuchagiza uungaji mkono wa kimataifa kwa nchi jirani za Syria ambazo zinawapa hifadhi.