Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola waanza operesheni zake kwa dharura

Harakati za kujikinga dhidi ya Ebola. (Picha@WHO)

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola waanza operesheni zake kwa dharura

Kufuatia mkutano maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, Katibu Mkuu Ban Ki Moon ametangaza kuunda ujumbe  wa dharura wa afya wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, UNMEER, jinsi ilivyoamuliwa kupitia azimio la Baraza Kuu.

Katika taarifa yake iliyotolewa ijumaa tarehe 19 Septemba, Ban Ki Moon ameeleza kwamba timu ya kwanza ya wafanyakazi inatakiwa kufika kwenye makao makuu ya ujumbe huo, mjini Accra, nchini Ghana, kuanzia jumatatu tarehe 22, Septemba.

Ameongeza kwamba malengo ya ujumbe huo yatakuwa ni kutokomeza maambukizi ya Ebola na kuzuia maambukizi mengine katika nchi zingine, kuhudumia wagonjwa, kusaidia katika utoaji wa huduma za kawaida na kuhakikisha utulivu katika nchi zilizoathirika.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kwamba, wakati mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, David Nabarro, ataendelea kutoa ushauri wake, atateua mwakilishi maalum kwa ajili ya kuongoza ujumbe huo, kwa kushirikiana na WHO.