Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sura ya dunia inabadilika: tunapaswa kustahamili

Watu wakivinjari katika moja ya miji huko barani Asia. (Picha: UN /Kibae Park)

Sura ya dunia inabadilika: tunapaswa kustahamili

Wakati idadi ya watu inaongezeka kwa kasi, hasa katika bara la Afrika, tunapaswa kukubali mabadiliko ya sura ya dunia, wamesema watalaamu wawili kutoka idara ya masuala ya kiuchumi na kijamii ya Umoja wa Mataifa, DESA.

Wakizungumza na wandishi wa habari mjini New York, wataalam hao wamesema mafanikio mengi yamepatikana katika kuendeleza haki na uzima wa watu  tangu mkutano wa kwanza kuhusu idadi ya watu na maendeleo uliofanyika mwaka 1994, lakini ahadi nyingi zilizotolewa wakati ule hazijatimizwa, hasa kwa upande wa usawa baina watu na nchi.

Thomas Grant, mkuu wa idhaa wa uratibu wa kisiasa na masuala ya mawasiliano baina mashirika ya Umoja wa Mataifa, amesema idadi ya watu imeongezeka na watalaamu wanakadiria kwamba itafikia Bilioni 9.6 ifikapo 2050, kasi kubwa ya ongezeko ikitokezea Afrika na Asia, wakati idadi ya watu inatarajia kupungua katika baadhi ya nchi zilizoendelea, na uhamiaji ukitarajiwa kuwa suluhu ya tatizo hilo.

(Sauti ya Grant)

 “Katika kipindi cha miongo mitatu ijayo, idadi ya watu itapungua katika zaidi ya nchi 40. Kwa baadhi ya nchi za Ulaya, itatokea katika miaka mitano tu ijayo. Wakati huo huo, idadi ya wazee inaongezeka: kuwezesha wazee na kuwapatia haki zao za kibinadamu na kuwasaidia kushirikiana kikamilifu katika jamii inapaswa kupewa kipaumbele. Dunia inabadilika na tunapaswa kujifunza kustahamiliana na kukubali kuwa na watu tofauti”  

Suala zima la idadi ya watu na jinsi ya kulipatia kipaumbele katika ajenda ya maendeleo endelevu ya baada ya mwaka 2015 litaangaziwa katika mkutano maalum utakaofanyika tarehe 22 septemba mjini New York.