Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya walinda amani Mali: Ban, Baraza la Usalama walaani

Picha ya @MINUSMA

Vifo vya walinda amani Mali: Ban, Baraza la Usalama walaani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani vikali mashambulizi dhidi ya walinda amani yaliyotokea tarehe 18 Septemba katika mkoa wa Kidal kaskazini mwa Mali na kusababisha vifo vya walinda amani watano kutoka Chad ilhali wengine watatu wakijeruhiwa.

Tangu kuanza kwa mkataba wa ujumbe wa umoja wa Mataifa wa kulinda amani, Mali, MINUSMA Julai 2013, walinda amani 21 wameuawa na wengine 84 wamejehuriwa katika mashambulizi na ajali zilizosababishwa na vilipuzi vilivyotegwa ardhini.

Katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa, Katibu Mkuu amewaomba wawakilishi wa vikundi vilivyojihami wanaokutana mjini Algiers, Algeria, kuchukua hatua kulingana na ahadi zao za kuzuia mashambulizi kama hayo yanayolenga Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, wamachama wa Baraza la Usalama wametoa taarifa yao ya kulaani pia mashambulizi hayo, wakipeleka rambirambi zao kwa familia za wahanga na serikali ya Chad na kurudia umuhimu wa kupambana na ugaidi na vitisho vyote vya amani ya kimataifa.