Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yoko Ono ana matumaini ya amani

UN Photo/Mark Garten)
Yoko Ono, mke wa mwimbaji John Lennon aliyeuawa mwaka 1980. Picha ya

Yoko Ono ana matumaini ya amani

Umoja wa Mataifa ukijiandaa kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani, tarehe 21 Septemba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewaomba watu wote wanaoshiriki katika mapigano waweke silaha chini kwa siku hii.

Maher Nasser, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa, amezungumza na Balozi Mwema wa Umoja wa Mataifa, msanii na mwanaharakati Yoko Ono, aliyekuwa mke wa mwimbaji maarufu John Lennon, maudhui ya mwaka huu ikiwa ni muziki.

Yoko Ono amesema ameamua kuupa Umoja wa Mataifa haki ya kutumia wimbo wa mume wake John Lennon, uitwao “Imagine”, ambapo alikuwa anawaomba raia kuwaza dunia yenye amani, kwa sababu wimbo huo umekuwa muhimu sana katika kuelewesha jamii kuhusu amani.

Amemwambia Maher Nasser kwamba ana matumaini makubwa kuhusu kutawala kwa amani duniani:

“ Nadhani duniani polepole tunaelekea vizuri. Najua tuko na subira na matumaini. Tulipooana mwaka 1969, hali ilikuwa mbaya sana. Hakuna mtu aliyekuwa anataka kusikia neno amani. Lakini sasa nadhani asilimia 99% ya watu duniani kwa kweli wanatumaini kuwa na amani. Kwa hiyo ni tifauti sana, na itapatikana.”

Halikadhalika, katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC unaandaa burudani ya muziki katika uwanja wa ndege wa Goma, tarehe 21 Septemba, ambapo miongoni mwa wasanii wanaotarajiwa kuimba jukwani ni mwimbaji wa Marekani Akon.