Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awa na mazungumzo na Rais Mutharika wa Malawi

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon na Rais Arthur Peter Mutharika, wa Malawi

Ban awa na mazungumzo na Rais Mutharika wa Malawi

Mjini New York, Marekani kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu Ban Ki-moon amekuwa na mazungumzo na Rais Arthur Peter Mutharika, wa Malawi ambapo wamejadili masuala kadhaa ikiwemo demokrasia nchini Malawi, amani na usalama barani Afrikana ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema katika mazungumzo hayo, Ban amempongeza Mutharika kwa kushinda uchaguzi nchini Malawi na vile ambavyo kipindi cha mpito wa demokrasia kilifanyika kwa amani na sasa kuna utulivu nchini mwake.

Halikadhalika amepongeza Malawi kwa mchango wake kwenye shughuli za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa hususan askari polisi wanawake na kumtia moyo aendelee na usaidizi huo.

Katibu Mkuu pia amemsihi Rais Mutharika kuendelea kuonyesha uongozi wake katika masuala yanayohusu Afrika huku akisifu maendeleo ya Malawi katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya Milenia.