Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanafunzi 300,000 warejea tena shuleni Gaza, Syria

Shareef Sarhan/UNRWA Archives

Wanafunzi 300,000 warejea tena shuleni Gaza, Syria

Karibu watoto 300,000 leo wameanza tena kurejea shuleni huko Ukanda wa Gaza na nchini Syria ikiwa mwaka mmoja sasa tangu kushuhudiwa kwa hali mbaya ya kiusalama na kusababisha shule nyingi kufungwa. George Njogopa na taarifa kamili.

(Taarifa ya George)

Katika Ukanda wa Gaza, machafuko yaliyoibuka miezi ya hivi karibuni yalitatiza mazingira ya shule na kusababisha shule nyingi kuchelewa kufunguliwa.

Kamishna na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Pierre Krähenbühl amesema kuwa hatimaye watoto hao sasa wameanza kuona nuru mpya baada ya kupita kipindi cha siku 50 chenye kihoro na mashaka makubwa.

Amesema mapigano hayo yalisababisha uharibifu mkubwa ikiwamo vifo, kuharibika kwa miundo mbinu na mali nyingine. Amesema kuwa kiasi cha watoto 240,000 wamefanikiwa kuliripoti katika shule zinazoratibiwa na shirika hilo zipatazo 252.

Awali shule nyingi katika Ukingo huo wa Gaza zilitumika kutoa hifadhi kwa waathirika wa mapigano.

Mapema akizungumza kutoka Damascus nchini Syria, kijana mmoja mwenye umri wa miaka 15 alisema kuwa kwake imekuwa furaha kubwa kwa kufanikiwa kurejea tena shuleni kwani anaona kuwa sasa ndoto yake ya

kuwa mhandisi inaweza kutimia.

Ameongeza kwamba ndoto yake kubwa ni kusaidia familia yake pamoja na majira yake kujenga mazingira bora ikiwemo nyumba za kisasa.