Baraza la Usalama lalani mauaji ya Haines
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali mauaji ya
mfanyakazi wa misaada ya kibinaadamu wa Uingereza Bw David Haines,
yaliyofanywa na kundi la ISIS.
Bwana Haines ni mateka wa tatu mgeni kuchinjwa na kundi la ISIS, kundi
ambalo katika miezi ya karibuni limetanua udhibiti wake nchini Syria
na kaskazini mwa Iraq.
Wajumbe hao wa nchi 15 pia wametoa rambirambi kwa familia ya marehemu,
serikali ya Uingereza, pamoja na familia za watu wote walioathiriwa na
kundi la ISIS.
Pia baraza hilo limesisitiza haja ya kukusanya nguvu ya pamoja ili
kuvishinda vitendo hiovu vinavyofanywa na kundi hilo linalotishia
kuanzisha Dola ya Kiislamu. Juzi usiku kundi la ISIS lilitoa video
inayoonesha Haines akichinjwa.