Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mladenov akaribisha amri ya Waziri Mkuu Iraq kusitisha mashambulizi

Nikolay Mladenov@Picha/UNAMI

Mladenov akaribisha amri ya Waziri Mkuu Iraq kusitisha mashambulizi

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu nchini Iraq, Nickolay Mladenov, amekaribisha hatua ya Waziri Mkuu na Kamanda wa Majeshi nchini humo Haider al-Abadi ya kuamuru kusitishwa kwa mashambulizi ya angani kwenye maeneo yanayokaliwa na raia, yakiwemo yale ambayo bado yamedhibitiwa na wanamgambo wanaotaka kuanzisha dola la Kiislamu, ISIL.

Mladenov amekaribisha pia ahadi ya Bwana al-Abadi ya kuwalinda raia, na kupongeza serikali ya Iraq na ile ya Jimbo la Kurdistan na viongozi wa kidini na jamii za wenyeji wanaotoa msaada wa makazi, chakula na matibabu kwa watu waliolazimika kuhama makwao.

Amesema Iraq inakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu, huku idadi ya watu waliolazimika kuhama ikiwa inaongezeka kwa kiasi kikubwa. Amesema watu hao wanahitajika kupewa hifadhi salama kulingana na haki zao za binadamu, akiongeza kuwa ulinzi wa raia na kuhakikisha usalama wao ni suala la kipaumbele kwa Umoja wa Mataifa.