Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya vijana nchini Iraq hawataweza kuanza shule sababu ya vita

watoto wakicheza kwenye kambi za wakimbizi nchini Iraq. Picha ya UNICEF Iraq

Maelfu ya vijana nchini Iraq hawataweza kuanza shule sababu ya vita

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bokova amesema maelfu ya watoto na vijana nchini Iraq wako hatarini kushindwa kujiandikisha shuleni mwaka huu kwa sababu ya vita, akiongeza kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kujali hatma ya watoto hao na kuiwekea kipaumbele elimu yao.

Kwa mujibu wa UNESCO, nusu ya raia wa Iraq wako na umri wa chini ya miaka 20, na mzozo unaoendelea nchini humo umeathiri zaidi ya watoto na wavulana 500,000 ambao wangepaswa kwenda shuleni.

Amesema wengi wao walishindwa kufanya mtihani wa mwisho wa mwaka mwezi Juni na watashindwa kuendelea na shule mwaka huu. Bi Bokova amesema zaidi ya hayo, shule nyingi zinatumika kama kambi kwa waliokimbia mapigano.

Shirika la UNESCO, kupitia ufadhili wa Saudi Arabia, linatoa mafunzo ya ziada kwa wanafunzi walioacha shule kwa muda kwa sababu ya vita, pamoja na nafasi za masomo ya chuo kikuu kwa wanafunzi wenye umri wa kati ya miaka 18 na 25.