Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tabaka la Ozoni kurejea hali yake ya kawaida- WMO

UN Photo/Kibae Park
uchafuzi wa hali ya hewa husababisha kumomonyoka kwa tabaka la ozoni na kubadilika kwa tabianchi. Hapa ni Toronto, nchini Canada. @

Tabaka la Ozoni kurejea hali yake ya kawaida- WMO

Tabaka la Ozone linalotulinda na miyonzi mikali ya jua liko kwenye mkondo wa kurejea hali yake ya kawaida, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na Shirika la Hali ya Hewa Duniani WMO na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira, UNEP.

Utafiti wa wanasayansi unatarajia kwamba, ifikapo 2050, hakutakuwa tena na penyo kwenye tabaka la ozoni, isipokuwa kwenye bara la Antartica na hivyo visa milioni 2 vya saratani ya ngozi vitazuiliwa.

Geir Braathen, afisa wa sayansi wa WMO amefafanua zaidi alipozungumza na redio ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva,

“ Kwa kuwa gesi hizo zinazoharibu Ozone hazizalishwi tena na hazitumiki tena, ina maana kwamba gesi hizo zitapungua angani. Mwelekeo ni polepole, lakini zinapungua kwa kasi ya asilimia moja kila mwaka. Kwa hiyo hata kama unaenda polepole, mwelekeo ni mzuri. Hatimaye, ifikapo 2050 takriban, tunatumai kwamba tabaka la ozone litakuwa limerejea hali yake, angalau katika maeneo yote ya dunia isipokuwa kwenye ncha ya Kusini”

Matokeo hayo yamepatikana kutokana na hatua zilizochukuliwa na nchi wanachama baada ya kusaini makubaliano ya Montreal, mwaka 1987, ili kudhibiti matumizi ya gesi zinazochangia kumomonyoa tabaka la ozone.

Michel Jarraud, Katibu Mkuu wa WMO amesema mafanikio hayo ya kuridhisha moyo yanapaswa kutupa moyo ili kukabiliana na changamoto zingine za mabadiliko ya tabianchi.