Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na Obama wajadili Ebola, mabadiliko ya tabianchi na Ukraine

UN Photo/NICA
Picha:

Ban na Obama wajadili Ebola, mabadiliko ya tabianchi na Ukraine

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekuwa na mazungumzo kwa njia ya siu na Rais Barack Obama wa Marekani ambapo wamejadili suala la Ebola, Ukraine na mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa tarehe 23 mwezi huu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephan Dujarric amesema kuhusu Ebola wamezungumzia jinsi ya kuongeza kasi ya kushughulikia ugonjwa huo unaozidi kuenea kwenye baadhi ya maeneo Afrika Magharibi.

(Sauti ya Dujarric)

"Katibu Mkuu amemtaarifu Rais Obama kuwa amepanga kuitisha kikao cha ngazi ya juu wakati wa vikao vya Baraza Kuu ili kuangazia mahitaji na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kutoka kwa serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na hata taasisi za kitaaluma.”

Halikadhalika amesema Ban amekaribisha jitihada za kujenga ushirika mpaka katika kudhibiti vitisho vinavyotokana na makundi yenye misimamo mkali yanayozidi kushikilia maeneo huko Syria na Iraq.

Pia amemshukuru Rais Obama kwa jitihada za Marekani za kusaidia wanaohitaji misaada ya kibinadamu huko Iraq hususan kwenye maeneo yasiyofikika.

Kuhusu Ukraine wamejadili umuhimu wa mfumo thabiti wa kufuatiali makubaliano ya sitisho la mapigano mashariki mwa nchi hiyo.