Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Moringa, zao la kiasili kwa mwezi Septemba, chanzo cha Vitamini na madini:FAO

Majani ya mmea uitwao Moringa. (Picha-FAO)

Moringa, zao la kiasili kwa mwezi Septemba, chanzo cha Vitamini na madini:FAO

Katika utambuzi wake zao la asili kila mwezi, wakati huu wa mwaka wa kimataifa wa kilimo cha familia, Moringa umetambuliwa kuwa zao la asili kwa mwezi Septemba huku Shirika la Chakula na Kilimo duniani likieleza kuwa ni chanzo cha Vitamini A, B na C pamoja na madini.

Tovuti ya FAO imesema Moringa Oleifera kama ujulikanavyo kitaalamu ni mmea wa asili kwa nchi za Kusini mwa bara la Asia lakini sasa aina Tisa za mmea huo zimeenea hadi Masahriki mwa Ethiopia, Sudan, Somalia na maeneo ya kaskazini mwa Kenya.

FAO inasema sehemu zote za mmea huo kuanzia, gome, majani, mbegu, mizizi hadi matawi yanalika na ni chanzo kizuri cha virutubisho kwa mwili wa binadamu.

Mathalani imesema majani yake huliwa mabichi au yakikauka hupondwa na kuwa unga unga, ilhali mbegu zake zaweza kuliwa mbich au kwa kupikwa bila kusahau mafuta yake.

FAO pamoja na kuelezea aina mbali mbali za mapishi ya Moringa kwenye tovuti yake, imesema kilimo cha Moringa kina manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wakulima wadogo kwani mmea huo unastahimili ukame, chanzo cha virutubisho vya afya kwa familia na miti yake huzuia mmomonyoko wa ardhi.