Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apigia debe ukarimu na kujitolea kwenye Siku ya Usamaria Wema

Siku ya Usamaria wema: Picha ya Maktaba ya UM

Ban apigia debe ukarimu na kujitolea kwenye Siku ya Usamaria Wema

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Usamaria Wema, Katibu Mkuu wa Moja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema usamaria wema una nafasi kubwa katika kazi ya Umoja wa Mataifa na mashirika yake.

Ban amesema usamaria wema unaweza kuchukua mfumo mbali mbali kama vile  kutoa muda na huduma ya kitaaluma ya moja kwa moja, mchango wa fedha binafsi, makampuni au kutoa misaada.

Katibu Mkuu amesema ukarimu na usamaria wema bila matarajio ya kunufaika unaweza kuleta mabadiliko  katika ustawi wa binadamu.

Halikadhalika, Ban ameelezea kuwa wakati huu mgumu wa kiuchumi, ukarimu unachukua nafasi muhimu katika jitihada za kimataifa za kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia na utekelezaji wa ajenda kabambe ya baada ya mwaka wa 2015.

Katibu Mkuu amekiri kuwa, japo kujitolea hakutachukua nafasi ya pesa za umma, lakini bado ni mchango mkubwa sana.

Ban amesema anakaribisha maadhimisho ya pili ya Siku ya Kimataifa ya usamaria wema,  iliyotangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika mpango wa ubalozi wa Hungary, sanjari na maadhimisho ya miaka ya kifo cha Mama Teresa, ambaye maisha na kazi nzuri kwa baadhi ya maskini na wanaoishi katika mazingira magumu na kwa ubinadamu  umekuwa kama msukumo mkubwa sana.