Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaitaka Iraq kuchunguza mauaji

Nikolay Mladenov@Picha/UNAMI

UN yaitaka Iraq kuchunguza mauaji

Umoja wa Mataifa umeitaka mamlaka nchini Iraq kuendesha uchunguzi wa umma na wa wazi kuhusu hatma ya mamia ya  askari waliouwawa pamoja na wafanyakazi wengine wa kijeshi wa kambi iitwayo Speicher ambayo ilitvamiwa na wanamgambo wa kikundi cha kiislamu chenye silaha kiitwacho Islamic State of Iraq na Levant mnamo June 12 , 2014.

(Taarifa zaidi na George Njogopa)

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Nikolai Mladenov, waasi hao ambao wamekuwa wakipigana kutaka kuanzishwa kwa nchi yenye kufuata misingi ya kidini walifanya mauaji ya halaiki kwa mamia ya askari na watumishi wengine jeshini.

Mwakilishi huyo amesema kuwa ushahidi wa awali unaonyesha kuwa kiasi cha askari 1,700 walinyongwa na waasi hao ambao pia wanadaiwa kuendesha vitendo vya kikatili katika maeneo mbalimbali kutokana na picha walizozituma kwenye mitandao.

Bwana Mladenov amesisitiza kuwa Iraq inapaswa kuchukua hatua zote zinazowezekana ili kufichua ukweli kuhusu kile kilichotendeka kwenye kambi hiyo.