Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi wa Sudan Kusini wana haki ya amani na ustawi: Mkuu mpya UNMISS

Mwakilishi mpya wa Katibu Mkuu wa UM nchini Sudan Kusini, , Ellen Margrethe Løj akizungumza na waandishi wa habari. (Picha: UNMISS / JC McIlwaine)

Wananchi wa Sudan Kusini wana haki ya amani na ustawi: Mkuu mpya UNMISS

Mwakilishi mpya wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudani Kusini, Ellen Margrethe Løj wa Denmark amesema wakazi wa nchi hiyo wanahitaji amani kwa hiyo mapigano lazima yasitishwe ili waweze kuwa na imani ya kurejea makwao.

Bi. Løj  amesema hayo baada ya kuwasili Juba, mji  mkuu wa Sudan Kusini ambapo pia atakuwa mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS.

Amesema kwenye kambi za UNMISS kuna zaidi ya wakimbizi Laki Moja, kando ya zaidi ya Milioni Moja waliosaka hifadhi maeneo mbali mbali nchini Sudan Kusini kutokana na mapigano yanayoendelea kwenye makazi yao.

“Wananchi wa Sudan Kusini walipambana vikali kwa ajili ya uhuru wan chi yao na hivyo naamini kwa dhai kuwa kila mmoja wao na raia yeyote popote pale duniani ikiwemo Sudan Kusini ana haki ya mustakhabli bora. Naamini kwa dhati kuwa watoto wenu wa kike na wa kiume watakuwa na fursa ya kupanga maisha yao na kufikia uwezo wao na siyo kuwa na hofu iwapo watauawa kesho au watalala njaa.”

Mkuu huyo mpya wa UNMISS anachukua nafasi iliyoachwa na Ellen Johnson wa Norway aliyemaliza muda wake tarehe Saba Julai mwaka huu.