Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asikitishwa na shambulio dhidi ya walinda amani wa Chad huko Mali

Picha@UM/Marco Dormino

Ban asikitishwa na shambulio dhidi ya walinda amani wa Chad huko Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameeleza masikitiko yake juu ya vifo vya askari wanne wa Chad vilivyotokea mapema Jumanne huko Kaskazini mwa Mali baada ya gari lao kulipuliwa mapema Jumanne.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema tukio hilo kwenye barabara moja huko Kidal limetokea baada ya kilipukaji kulipua gari hilo lililokuwa limebeba askari wanaohudumu kwenye vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA ambapo walinda amani wengine 15 wamejeruhiwa.

Ban amelaani tukio hilo ambalo ni miongoni mwa mfululizo wa matukio dhidi ya watendaji wa Umoja wa Mataifa na wakandarasi wake kwenye eneo la Kidal tangu wiki iliyopita.

Matukio mengine ni lile la shambulizi la kombora kwenye kambi ya MINUSMA na kilipuzi cha tarehe 29 Agosti kilichosababisha walinda mani Tisa wa Chad kujeruhiwa.

Katibu Mkuu amesema mashambulizi hayo kamwe hayatazuia azma ya Umoja wa Mataifa kusaidia wananchi wa Mali kusaka amani ya kudumu.

Ametuma rambirambi kwa familia za walinda amani waliofariki dunia pamoja na serikali ya Chad huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.