Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wengi wanazidi kukimbia mapigano Ukraine:UNHCR

Familia kutoka Ukraine baada ya kuwasili Kyiev kwa njia ya reli © UNHCR/I.Zimova

Wengi wanazidi kukimbia mapigano Ukraine:UNHCR

Barani Ulaya, kiwango cha watu wanaokosa makazi katika eneo la Mashariki mwa Ukraine kimeripotiwa kuongezeka maradufu katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita huku mamia ya watu wakiendelea kuyakimbia maeneo yao kwa hofu  ya mapigano, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Wakimbizi, UHNCR kama anavyoripoti George Njogopa.

(Taarifa ya George)

Kulingana na takwimu zilizotolewa na UNHCR hadi kufikia Septemba mosi mwaka huu idadi ya watu waliokosa makazi ilifikia 260,000  ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na ile ya awali iliyokuwa 117,000.

Kuna wasiwasi kwamba idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi kwa vile familia nyingi bado hazijasajiliwa. Hali mbaya zaidi katika miji ya Donetsk na Luhansk ambako ndiko kunakoshuhudiwa idadi kubwa ya waathirika.

UNHCR inasema kuwa kiasi cha watu zaidi ya milioni ambao ni raia wa Ukraine wamevuka mpaka na kuingia Urusi tangu kuanza kwa machafuko hayo mwanzoni mwa mwaka huu.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Antonio Guterres ameonya kuhusu kutokea maafa zaidi katika siku za usoni ikiwemo kuzorota kwa misaada ya kibinadamu iwapo mzozo huo utakosa ufumbuzi.  Adrian Edwards  ni msemaji wa UNHCR

(Sauti ya Adrian)

Kutokana na kukosekana kwa usalama, watoaji wa misaada ya kibinadamu wameshindwa kutathmini hali ilivyo kwa watu wanaokosa makazi katika jimbo la Luhansk . UNHCR ina mpango wa kutuma ujumbe wake wiki hii pale hali itaporuhusu. Hadi kufikia Septemba mosi watu zaidi ya Milioni Mbili walikuwa wamesalia kwenye maeneo yenye mapigano na hii ni kwa mujibu wa serikali ya Ukraine".

Hadi sasa kiasi cha raia 4,000 waUkraine wameomba hifadhi katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.