Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu lakutana kuhusu Iraq: ISIL yamulikwa

Kikao cha Baraza la haki za binadamu. (Picha-UM)

Baraza la haki za binadamu lakutana kuhusu Iraq: ISIL yamulikwa

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeelezwa kuwa kikundi cha waislamu wenye msimamo mkali nchini Iraq, ISIL pamoja na washirika wake kinakiuka haki za binadamu za wakazi wa Kaskazini mwa nchi hiyo katika kiwango kisichoweza fikiriwa, jambo ambalo linaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.

Akihutubia kikao maalum cha Baraza hilo kilichofanyika Geneva siku ya Jumatatu mahsusi kwa ajili ya Iraq, Naibu Kamishna wa Haki za binadamu Flavia Pansieri ametaja vitendo hivyo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kuwa ni pamoja na mauaji, mateso, utekaji nyara, utumwa, ukatili wa kingono na vipigo na kuzingirwa kwa jamii nzima kwa misingi ya kabila au Imani zao.

Bi. Pansieri amesema ISIL inajihusisha na utekaji nyara, na utumikishaji wa wavulana kwenye vikosi vyao akiongeza kwamba baadhi yao walitumiwa kama ngao kwenye mapigano au kulazimishwa kutoa damu kwa ajili ya wapiganaji waliojeruhiwa.

Ametaja makundi madogo yanayokumbwa na udhalimu huo unaoelekea kuwa mauaji ya kutokomeza makabila au waumini wa Imani hizo kuwa ni pamoja na wakristu, Wayazidi na washia.

Naibu Kamishna huyo amesema ofisi yake ina taarifa za vitendo vya ukiukaji haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu vinavyoweza kuw ani uhalifu wa kivita, vitendo vilivyofanywa na jeshi la usalama la Iraq na vikundi vilivyojihami.

(Sauti ya Pansieri)

 “Yaonekana kuwa wanamgambo wa ISIL wanatekeleza vitendo vyao vilivyoenea vya manyanyaso dhidi ya jamii za makabila au imani Fulani ya dini, na hivyo kuwayima haki yao ya msingi ikiwemo haki ya kuishi na uhuru wa kuabudu. Halikadhalika kuwanyima haki ya utambulisho wao na kuwalazimisha kutangatanga wakiwa na woga kwenye maeneo hatarishi. Vitendo hivyo ni ukatili dhidi ya utu na ubinadamu. Ijapokuwa mgogoro huu umepunguza kwa kiwango kikubwa wigo wa eneo linalodhibitiwa na serikali ya Iraq,bado serikali ina wajibu wa msingi wa kulinda raia kweny eneo lake na lazima ijitahidi kutekeleza wajibu huo.”

Baraza hilo la haki za binadamu linatarajiwa kupitisha azimio la kuitaka ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ipeleke ujumbe nchini Iraq kuchunguza madai ya ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu unaofanywa na ISIL na vikundi shirika vya kigaidi. Lengo la uchunguzi huo ni kuhakikisha watakaobainika kuhusika wanawajibishwa ipasavyo.