Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atawazwa Chifu wa heshima huko Samoa

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon (katikati) baada ya kutawazwa kuwa chifu wa kijiji cha Saleapaga, huko Samoa. (Picha:Daniel Dicknson)

Ban atawazwa Chifu wa heshima huko Samoa

Huko Samoa siku ya Jumapili Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amepatiwa cheo cha juu kabisa cha heshima kinachopewa machifu wa ngazi ya juu kabisa wa vijiji nchini humo.

Ban amepatiwa jina la Tupua au Chifu wa Saleapaga, kijiji kimoja kilichopo Kusini-Mashariki mwa Samoa, kijiji ambacho kilisambaratishwa na Tsunami ya mwaka 2009.

Mwandishi wetu aliyeko Samoa anasema kuwa ni nadra sana kwa cheo hicho kupatiwa wageni wa ngazi ya juu kutoka nje ya Samoa.

Baada ya kutawazwa na kuvalia vazi la kitamaduni liitwalo Siapo Lavalava ambalo ni aina ya msuli na kitambaa chenye manyoya kuzunguka kichwa chake, Katibu Mkuu alizungumza na kutoa shukrani zake na kwamba yuko tayari kutekeleza wajibu wake kama Chifu wa Samoa.

(Sauti ya Ban)

Ni heshima kubwa kwangu mimi kutembelea Samoa wakati huu. Nashukuru sana kwa kunibariki, kuniheshimu na kunipatia jina la Tupua. Ni heshima kubwa. Nitazingatia desturi zote na cheo hiki huku nikitekeleza majukumu yangu ya Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.”

Wakazi wa kijiji cha Saleapaga walijenga upya kijiji chao maeneo ya nyanda za juu mbali kabisa kutoka eneo la pwani ili kujikinga dhidi ya Tsunami inayoweza kutokea siku za usoni.

Katibu Mkuu Ban yuko Samoa ambako anashiriki mkutano wa nchi za visiwa vidogo zinazoendelea, SIDS ambako washiriki kutoka zaidi ya nchi 100 watajadili jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na masuala mengine yanayokabili nchi za SIDS.