Wahanga wa ajali ya helikopta Bentiu wasafirishwa

29 Agosti 2014

Maiti za raia watatu wa Urusi waliokufa kuafuatia kutunguliwa kwa helikopta ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudani Kusini UNMISS wamesafirishwa  kwenda Urusi kwa mazishi.

Shughuli ya kuaga maiti hao imefanyika katika uwanja wa ndege wa Juba ambapo kaimu mkuu wa ujumbe wa UNMISS Toby Lanzer amesisistiza kuwa uchunguzi wa chanzo halisi cha tukio hilo unaendelea.

(SAUTI LANZER)

"Tumedhamiria kuhakikisha tunafahamu mazingira kamili yaliyosababisha maafa haya . Timu yetu imeanza uchunguzi wa awali, na tutaendelea kufanya kazi kuhakiisha kuwa taarifa zote za tukio hili la kuogofya zinawekwa hadharani haraka iwezekanavyo kwa uwazi mkubwa uhakika."

Kwa upande wake rubani mkuu wa shirika la ndege la UT linalomiliki helikopta hiyo Oleg Belevikin amesema jumuiya ya kimataifa imepoteza watu muhimu waliojikita katika kurejesha amani

(SAUTI YA OLEG BELEVIKIN)

"Tumepoteza watu wazuri na watu ambao walikuwa na mipango ya mustakabali mwema kama tuliyonayo. Watu waliokuja hapa kusaidia amani duniani. Hili ndilo jukumu kuu la Umoja wa Mataifa na kwa kila mtu. Wapendwa wote waliofariki walikuwa na familia na watoto ambao waliokuwa wanawasubiri warudi nyumbani."

Katika ajali hiyo ya jumanne mjini Bentiu jimbo la Unity nchini Sudani Kusini wiki hii mtu mmoja alijeruhiwa na anaendelea kupata matibabu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter