Sekta binafsi waanza kukutana kabla ya kuanza kwa SIDS Jumatatu huko Samoa

Picha: UN SIDS.

Sekta binafsi waanza kukutana kabla ya kuanza kwa SIDS Jumatatu huko Samoa

Wawakilishi wa kampuni kubwa za biashara kutoka sehemu mbali mbali duniani wanakusanyika huko Kisiwa cha Samoa  kujadili namna bora ya kusaidia maendeleo ya mataifa ya visiwa vidogo yanayoendelea, SIDS.

Nchi hizo zina tabia zinafanana ikiwemo ukubwa wa maeneo  yao, umbali kutoka maeneo mengine na hata ukosefu wa rasilimali na miundombinu duni na hivyo kuonekana kuwa hatarini kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili.

Mkutano wa SIDS unaanza tarehe Mosi mwezi ujao ambapo wawakilishi hao kutoka sekta binafsi wameanza kukutana.

Gyan Chandra Acharya ni  Msaidizi wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo ya nchi za visiwa vidogo na anasema sekta binafsi ina majukumu muhimu.

(Sauti ya Acharya)

 "Kama ukiangalia changamoto zao hasa kiuchumi; wana idadi ndogo sana ya watu, wapo mbali na masoko makubwa; gharama ya mafuta ni ya juu sana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa ni makubwa. Hivyo tunaamini kuna ulazima wa kuwepo na mkakati unaohusisha wadau mbalimbali ili kupatia ufumbuzi tatizo hili. Serikali ina jukumu muhimu., sekta binafsi ina jukumu lake na mashirika ya kiraia halikadhalika.”

Umoja wa Mataifa umetambua visiwa vidogo 50 vilivyoko bahari ya Pasifiki naile ya Hindi kama  SIDS.