Idadi ya vifo vya raia Ukraine yafikia kiwango cha juu

29 Agosti 2014

Ripoti mpya ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa idadi ya watu wanaouawa Mashariki mwa

Ukraine imeongezeka mara tatu ndani ya mwezi mmoja uliopita wakati serikali na makundi yaliyojiami yakiongeza matumizi ya silaha nzito katika maeneo yenye wakazi wengi. Taarifa kamili na Abdullahi Boru.

(Taarifa ya Abdulahi)

Ripoti hiyo inasema kila siku watu 36 wanauawa kwa wastani ikilinganishwa na watu 11 mwezi uliopita. Imesema kati ya mwezi Aprili na Agosti huu takribani watu  2600 wameuawa mashariki mwaUkraine.   Ripoti inasema makundi yaliyojiami yanalenga raia ambao wanatumia maeneo salama yaliyowekwa ili kuondoka kutoka miji ya Luhansk na Donetsk.

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navy Pillay amesema kuna umuhimu wa kumaliza mapigano na vurugu Mashariki mwaUkraine kabla ya raia wengi zaidi kuathiriwa, kulazimika kuhama makwao ama kukumbana na hali mbaya mno katika maeneo ya vita.

Mkuu wa  tawi la ofisi ya Umoja wa Mataifa inayo shughulikia haki za Binadamu Marekani, Ulaya na Asia ya Kati. Gianni Magazzeni, amesema,

(Sauti ya Magazzeni)

 "Kuna hofu imetanda na woga kwenye maeneo yanayodhibitiwa na vikundi vilivyojihami. Hilo halijabadilika nap engine hali ni mbaya zaidi. Kadri hali inavyozidi kudorora kwenye maeneo raia wanataka kuondoka kwenye mizozo, wanashindwa kufanya hivyo na kuna maeneo imeripotiwa kuwa raia wanauawa pindi wanapopita maeneo salama yaliyotengwa. Lazima suala la ukwepaji sheria liondolewe na watekelezaji wawajibishwe. Na kuna umuhimu wa kuchukua hatua zaidi kulinda raia hususan kwa sababu ya kuongezeka kwa operesheni za mapigano kwenye baadhi ya maeneo ya  mashariki.”

Ripoti inasema serikali imekamata zaidi ya watu 1,000 miongoni mwao ni viongozi wa mitaa, maafisa wa polisi na raia kwa shutma ya kushiriki katika shughuli za kigaidi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud