Migogoro na vifo duniani huninyima usingizi: Pillay

29 Agosti 2014

Migogoro inayoendelea duniani na kusababisha maisha ya watu kupotea, majeruhi na watoto kutumikishwa  inaninyima usingizi.

Ni kauli ya Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navy Pillay aliyoitoa wakati akihojiwa na Elisabeth Philip wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa kuelezea mambo aliyokutana nayo wakati wa uongozi wake unaofikia ukomo mwisho wa mwezi huu.

Bi. Pillay amesisitiza kitendo cha watoto kuhusishwa katika migogoro ni  moja ya mambo yaliyokuwa yanampatia wakati mgumu zaidi.

(SAUTI PILLAY)

“Kinachonigusa zaidi ni pale watoto wanapouliwa na kujeruhiwa. Hawana hatia kabisa lakini hujikuta katika migogoro. Hakuna anayeweza kuhalalisha watoto kuwa wapiganaji. Hili hunipa wakati mgumu.”

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa haki za binadamu kadhalika amezungumzia juhudi za kutanzua mizozo na namna alivyojikita kuhakikisha utekelezaji wa haki za binadamu

(SAUTI YA PILLAY)

“Ningeweza kufanya zaidi kusaidia kuzuia mizozo kama ningaliweza. Nimetembelea nchi takribani 50 hadi 60. Kulikuwa na manufaa ya ziara hizo. Mathalani kuongea na asasi za kiraia katika nchi hizo, kuongea na wakuu wa nchi na viongozi waandamizi wakiwamo mawaziri na kutoa msaada ambao hasa ndiyo taaluma yetu katika kuangazia ukiukwaji wa haki za binadamu katika kusaida kubadilisha sheria, kutoa mafunzo kwa mahakama na  wetekelezaji wa sheria katika kutumia mifumo ya kuheshimu haki za binadamu.

Bi. Pillay amesema baada ya kustaafu atatutumia muda wake kuwa mtetezi wa haki za binadamu akiwa mapumzikoni jijini Durban Afrika Kusini nchi aliyozaliwa.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter