Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kinachoendelea Ukraine hakipaswi kufumbiwa macho: Baraza laelezwa

Jeffrey Feltman, Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama. (Picha:UN /Loey Felipe)

Kinachoendelea Ukraine hakipaswi kufumbiwa macho: Baraza laelezwa

Mazungumzo kati ya Rais Vladmir Putin wa Urusi na Petro Poroshenko wa Ukraine ambayo yalitia matumaini katika kumaliza mzozo unaoendelea yametiwa doa na mfululizo wa mapigano yaliyoripotiwa katika siku mbili zilizopita Kusini-Mashariki mwaUkraine.

Hiyo ni sehemu ya hotuba ya Mkuu wa Masuala ya siasa ndani ya Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman aliyoitoa mbele ya baraza la usalama wakati wa kikao cha dharura kilichoitishwa Alhamisi kuhusu Ukraine.

Feltman amenukuu ombi la Rais Poroshenko la kutaka dunia itilie maanani kinachoendelea Ukraine kwani madhara ya kinachotokea sasa kinavuka mipaka ya nchi hiyo na hata ukanda mzima.

Amesema vikundi haramu vilivyojihami vinavyoendesha shughuli zao huko Donetsk vinaripotiwa kuimarisha mapigano katika siku mbili zilizopita vikieneza mapigano hayo kwenye pwani ya kusini mwa Ukraine kuelekea bandari muhimu ya Mariupol.  Feltman akatoa angalizo.

(Sauti ya Feltman)

Hatuwezi kupuuza ripoti zinazotia wasiwasi mkubwa za madai ya kuhusika kwa jeshi la Urusi kwenye mapigano haya mapya. Iwapo itathibitika, itakuwa ni kinyume na sheria za kimataifa na katiba ya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa hauna njia huru ya kuthibitisha taarifa hizi na serikali ya Urusi imekataa kabisa ripoti hizo.”

Feltman amesema leo wamezungumza na balozi Apakan ambaye ni Mkuu wa jopo maalum la kufuatilia hali ilivyo kutoka shirika la ulinzi na ushirikiano la Ulaya, OSCE  ambaye amemweleza kuwa kwa sasa hakuna watendaji wao huko Mariupol na Novoazosk lakini wako mbioni kupeleka jopo hilo.

Hata hivyo Feltman amesema jambo muhimu sasa ni kubadilisha mwelekeo wa mapigano na kuondokana na mzozo huo ili kuwa na suluhu la kisiasa na mashauriano.