Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yawasilisha ICJ mzozo wa mpaka kati yake na Kenya

Jengo la mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ huko The Hague, Uholanzi. (Picha: UN/Rick Bajornas)

Somalia yawasilisha ICJ mzozo wa mpaka kati yake na Kenya

Serikali ya Somalia leo imewasilisha mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ huko The Hague, Uholanzi ombi la kutaka mahakama hiyo ichukua hatua juu ya mzozo wa mpaka wa baharini kati ya nchi hiyo na Kenya.

Katika ombi lake likiwa na viambatanisho kadhaa ikiwemo michoro ya ramani, Somalia imesema pande mbili hizo zimeshindwa kukubaliana juu ya eneo la mpaka rasmi kati yao kwenye bahari ya Hindi na hata jitihada za kidiplomasia zimeshindwa kuzaa matunda.

Kwa mantiki hiyo Somalia imetaka ICJ kwa misingi ya sheria ya kimataifa inaeleza bayana mpaka ulipo ikiwemo eneo la umbali wa maili 200 za baharini kutoka usawa wa ardhi.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu sheria ya bahari unasema kuwa iwapo nchi zilizoridhia mkataba huo zinashindwa kuafikiana kuhusu mpaka wa majini, basi zinaweza kuwasilisha suala hilo ICJ.

Somalia na Kenya ziliridhia mkataba huo mwaka 1989.