Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi wa ajali ya helikopta ya UNMISS waanza, UM wasema ni uhasama

MI-8 helikopta ilikodishwa na UNMISS. Picha: UNMISS / Martine Perret

Uchunguzi wa ajali ya helikopta ya UNMISS waanza, UM wasema ni uhasama

Uchunguzi wa ajali ya helikopta ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudani Kusini UNMISS iliyotunguliwa jumanne wiki hii umeanza huku UNMISS ikisema kitendo hicho cha kutunguliwa ni uhasama dhidi ya Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na waaandishi wa habari nchini Sudan Kusini hii leo Kaimu Mkuu wa UNMISS  Toby Lanzer amesema vifaa vya uchunguzi vimekusanywa tayari kuanza mara moja kwa hatua hiyo .

(SAUTI LANZER)

"Tunachukulia huu kama uhasama dhidi ya Umoja wa Mataifa. Ndege zinaruka hazianguki angani. Kwa sasa tuna kifaa maalum  cha taarifa yaani kasha jeusi, tuna kifaa cha kurikodia sauti za mwenendo wa ndege pamoja na bapa la kudhibiti mwenendo wa helikopta. Uchunguzi umeanza jana, uchambuzi unaendelea na siwezi kufafanua zaidi ya hilo."    

Kiongozi huyo wa UNMISS amefafanua kuhusu kusimamishwa kwa huduma za misaada ya kiutu katika mji wa Bentiu ulioko jimbo la Unity kulikotunguliwa helikopta hiyo.

(SAUTI LANZER)

"Ujumbe wa Umoja w Mataifa Sudani Kusini na shirika lake la kutoa misaada ya kibinadamu kupitia njia ya anga zimesitisha usafiri wa ndege mjini Bentiu tunatarajia kuzirejesha haraka iwezekanavyo."    

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu watatu raia wa Urusi na mmoja kujeruhiwa.