Kutunguliwa kwa helikopta ya UNMISS, Baraza lalaani vikali

27 Agosti 2014

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali kitendo cha kutunguliwa kwa helikopta ya ujumbe wa umoja huo Sudan Kusini, UNMISS siku ya Jumanne  ambapo watu watatu raia wa Urusi walifariki dunia na mmoja alinusurika hifo.

Taarifa ya Baraza hilo imekariri wajumbe wakituma rambirambi kwa wafiwa hao na kwa serikali ya Urusi huku wakimtakia ahueni majeruhi.

Wamesisitiza kuwa shambulio hilo ni ukiukwaji mkubwa wa makubaliano kuhusu masuala ya kijeshi yaliyotiwa saini Agosti Nane mwaka 2011 na pia yanakwaza operesheni za UNMISS.

Wamesihi kwa dhati UNMISS na serikali ya Sudan Kusini waanzishe haraka uchunguzi wa wazi wa tukio hilo wakisisitiza kuwa wahusika wafikishwe mbele ya sheria ili kuhakikisha kitendo cha aina hiyo hakirudiwi tena.

Halikadhalika wameomba UNMISS ichukue hatua za ziada zinazostahili kuhakikisah usalama wa operesheni zake za angani huko Sudan Kusini na kuripoti hatua hizo kwa Baraza hilo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter