Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yasisitiza haja ya kukabili mabadiliko ya tabia nchi ili kunusuru afya za wengi

Nembo ya WHO

WHO yasisitiza haja ya kukabili mabadiliko ya tabia nchi ili kunusuru afya za wengi

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema kuwa dunia inaweza kupiga hatua ya kuondokana na matatizo ya kiafya iwapo itachukukua jukumu la kulinda amazingira.

Shirika hilo limesema kuwa, kama kutawekwa umakini wa kukabiliana na matatizo ya tabia nchi kama vile kuanzisha sera zinazohimiza maendeleo endelevu basi kunaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watu wanaokumbwa na magonjwa yasababishwayo na uchafuzi wa mazingira.

Hayo yameelezwa na shirika hilo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa unaofanyika Geneva na kuwahusisha wataalamu zaidi ya 300 kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Mkutano huo unaojulikama kama afya na hali ya hewa pia unawajumuisha mawaziri, wakuu wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk.Margaret Chan alisema kuwa kunauhusiana mkubwa kati ya mabadiliko ya tabia nchi na afya ya binadamu.

Alisema kuwa hali yoyote ya mabadiliko ya tabia nchi ni kitisho kikubwa kwa afya ya binadamu hivyo alihimiza kuwekwa mikakati ya kukabiliana nayo.