Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sigara za kielektroniki zina madhara ziwekewe kanuni: WHO

Picha@UN WHO

Sigara za kielektroniki zina madhara ziwekewe kanuni: WHO

Ripoti mpya ya shirika la afya duniani, WHO imetaka kuwekwa kwa kanuni na taratibu za kimataifa katika matumizi ya sigara za kielektroniki na vifaa vinginevyo vinavyoonekana kuwa mbadala wa uvutaji tumbaku. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Msingi wa pendekezo hilo la kuwekwa kanuni za kudhibiti matumizi ya sigara za kielektroniki ni ushahidi uliobainisha kuwa matumizi yake yana madhara kwa afya ya umma tofauti na inavyodhaniwa.

WHO inataka udhibiti ili kutoa fursa kwa utafiti zaidi juu ya sigara hizo na pia kuzingatia matokeo ya tafiti zilizokwishafanyika.

Mkurugenzi wa WHO anayehusika na kinga dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Dokta Douglas Bettcher amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa madhara yako dhahiri.

(Sauti ya Dkt. Bettcher)

“Ushahidi unaonyesha kwamba wakati zinaonekana kuwa na madhara kidogo kulingana na sigara za kawaida, matumizi ya sigara za kielektroniki ni tishio kwa wavutaji vijana barurabu na kwa mtoto aliye tumboni kwa mama mjamzito. Pia kemikali zinazotoka kwenye sigara hizo zina madhara kwa wasiovuta au watu walioko eneo la karibu zinapovutwa.”

Kanuni zilizopendekezwa na ripoti hiyo ni kupiga marufuku sigara zote za kielektroniki zenye ladha ya matunda, pipi na pombe hadi pale itakapothibitika kuwa hazina mvuto kwa watoto na vijana barubaru.

Matumizi ya sigara za elektroniki ni moja ya ajenda ya mkutano wa Sita wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa kudhibiti amtumizi ya tumbaku utakaofanyika Moscow Urusi kuanzia tarehe 13 hadi 18 Oktoba mwaka huu.