Umoja wa Mataifa wakaribisha hatua za kwanza za ukaguzi Afghanistan, Eliasson asema ni muda wa kukubali matokeo

Fraidoon Poya / UNAMA
Ukaguzi wa kura nchini Afghanistan.

Umoja wa Mataifa wakaribisha hatua za kwanza za ukaguzi Afghanistan, Eliasson asema ni muda wa kukubali matokeo

Baada ya jopo la ukaguzi wa matokeo ya uchaguzi wa Urais nchini Afghanisan kutoa ripoti zake za kwanza, Jan Kubis, mkuu wa Ujumbe wa Mataifa nchini humo, UNAMA, amesema ni hatua muhimu katika kufikia ukweli.

Tume hiyo iliundwa baada ya wagombea wawili wa Urais Dkt Abdullah Abdullah na Dkt Ashraf Ghani kutoelewana juu ya matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Juni mwaka huu.

Umoja wa Mataifa umesaidia kusafirisha zaidi ya makasha 22,000 ya kura kutoka sehemu mbalimbali za nchi hiyo hadi Kabul ambapo watalaam wa uchaguzi wanaendelea kukagua.

Awali siku ya jumatatu, tarehe 25, Agosti, tume hiyo imetangaza kwamba kutoka masanduku 3,644 ya kura ya kwanza yaliyokaguliwa, asilimia 79 yamehakikishwa, mengine yakithibitishwa kuwa ya udanganyifu.

Wakati huo huo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, kwenye Makala aliyoandika leo katika gazeti la Huffington Post, amekaribisha jitihada za tume ya Afghanistan pamoja na timu za wagombea wawili walioshirikiana katika utaratibu huo. Amesema kazi zinakaribia kumalizika.

Cha msingi , amesema ni utashi wa wagombea kuheshimu matokeo ya ukaguzi huo. Wasipoelewana, kuna hatari kwa utengamano wa kiuchumi na uaminifu wa raia wa Afghanistan na mamlaka za serikali.

Amesema muda umefika kukubali matokeo ya uchaguzi na kujenga hatma ya matumaini kwa nchi ya Afghanistan.