Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vizuizi vya usafiri wa ndege changamoto kwa vita dhidi ya Ebola

Picha@WHO

Vizuizi vya usafiri wa ndege changamoto kwa vita dhidi ya Ebola

Uamuzi wa baadhi ya kampuni za ndege kusimamisha usafiri wao kutoka au hadi nchi zilizoathirika na Ebola ulikuwa hauna msingi wa uhakika, amesema Stephane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa.

Dujarric amewaleza waandishi wa habari mjini New York kuwa vizuizi hivyo havitasaidia kupunguza maambukizi wala havina uhusiano na jinsi Ebola inavyoambukizwa.

Amesisitiza kwamba Ebola haiambukizwi kwa njia ya hewa na kwamba mgonjwa asiye an dalili za Ebola hawezi kuambukiza wengine.

Hivyo amesema maambukizi yanaweza kudhibitiwa kwa kupima abiria kabla hawajapanda ndege, au baada ya kufika kwenye nchi nyingine na kwamba Shirika la Afya Duniani, WHO, linaweza kusaidia nchi zote kuimarisha mifumo yao ya udhibiti mpakani.

Aidha Dujarric ameeleza vizuizi vya usafiri wa ndege vinakumba mashirika mbali mbali yanayojitahidi kupambana na ugonjwa huo.

Mathalani vinakwamisha usafiri wa watalaam wa afya au usafiri wa  vifaa vya matibabu na zaidi ya yote  vizuizi hivyo vinaongeza vikwazo vya kiuchumi na kidiplomasia dhidi ya nchi hizo, na kuongeza unyanyapaa unaoathiri raia wao.