Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aendelea na harakati za kuleta suluhu ya kudumu huko Gaza

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon. (Picha-Maktaba-UM)

Ban aendelea na harakati za kuleta suluhu ya kudumu huko Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameendelea na jitihada zake za kusaka suluhu kwenye mzozo unaoendelea huko Ukanda wa Gaza ambapo leo amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema katika mazungumzo hayo wawili hao wamejadili mzozo wa Gaza ikiweo umuhimu wa pande zote husika kurejea kwenye mashauriano yatakayowezesha kusitishwa kwa mapigano chini ya uratibu wa Misri.

Ban amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kuunga mkono makubaliano yoyote yanayoweza kufikiwa.

Halikadhalika amemsihi Waziri Mkuu Netanyahu kurejea katika hali ya utulivu na kumtia moyo achukue hatua za kuwezesha jitihada zinazofanywa na Misri.

Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa pande hizo ambzo ni Palestina na Israeli kuwa na sitisho la kudumu la mapigano kwa minajili ya kurejea katika mashauriaono yenye maana kuhusu uwepo wa mataifa hayo mawili kwa pamoja.