Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mizozo ya kikabila Myanmar yasababisha maelfu kuhatarisha maisha yao baharini

Idadi ya watu wanaohatarisha maisha yao kwenye boti ya ushafirishaji haramu katika pwani ya Bengal kufuatia ghasia ya hivi karibuni katika jimbo la Rakhine, Myanmar. Picha: UNHCR Myanmar(UN News Centre)

Mizozo ya kikabila Myanmar yasababisha maelfu kuhatarisha maisha yao baharini

Mapigano ya kikabila kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar yamesababisha watu zaidi ya 87,000 kutumia njia hatari ya safari ya baharini ili kukimbia makazi yao.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR linasema idadi hiyo ni katika kiindi cha miaka miwili iliyopita na wamekuwa wakisafiri kupitia ghuba ya Bengal.

Wengi wao ni wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar wakijumuisha pia raia wa Bangladesh wanaokimbia makwao.

Mathalani mwaka huu pekee, UNHCR inakadiria kuwa zaidi ya wahamiaji 20,000 walifanya safari hiyo ya hatari kutoka Myanmar na Bangladesh kuelekea Thailand, Malaysia, Indonesia na kwingineko. Adrian Edwards msemaji wa UNHCR anaeleza kuwa wahamiaji hao huwalipa wasafirishaji haramu hadi dola 300 kwa safari hiyo kupitia ghuba ya Bengali.

(Sauti ya Adrian)

“Mambo haya mapya yanafanyika katika hali ya ukosefu wa mazingira salama ya wakimbizi kwenye eneo hili. Nchi kama vile Thailand, Malaysia na Indonesa hazijatia saini mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi na hazina mifumo ya kisheria ya kushughulikia wakimbizi. Wakimbizi wakiwa hawana kibali cha sheria cha kuishi, mara nyingi wanakuwa hatarini kukamatwa, kushikiliwa na hata kurejeshwa makwao kwa mujibu wa sheria za uhamiaji. Inafanya pia ajira halali isiwezekane na kusababisha watu wengi ikiwemo wanawake na watoto watumikishwe na kuwa katika mazingira hatarishi. Kuna ripoti pia zisizothibitishwa za vifo kutokana na magonjwa, joto, ukosefu wa chakula na maji pamoja na vipigo vya kupindukia pindi watu wanapojaribu kuondoka. Baadhi ya abiria wameripotiwa kujitosa baharini kutokana na kukata tamaa.”

UNHCR inasema zaidi ya wasaka hifadhi 7,000 na wakimbizi ambao wamesafiri kwa njia ya bahari wanashikiliwa maeneo mbali mbali ya Kusini Mashariki mwa Asia ikiwemo zaidi ya 5,000 nchini Australia au kwenye vituo vyao ya muda vilivyoko Nauru na Papua New Guinea.