Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lapitisha azimio kuhusu amani na usalama duniani

UN Photo/Paulo Filgueiras
Baraza la Usalama. Picha:

Baraza la usalama lapitisha azimio kuhusu amani na usalama duniani

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu ulinzi wa amani na usalama duniani na kupitisha azimio ambalo pamoja na mambo mengine linasisitiza umuhimu wa kuangazia viashiria vya mizozo. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Balozi Mark Lyall Grant Rais wa Baraza la usalama akitangaza kupitishwa kwa kauli moja kwa azimio hilo namba 2171. Azimio linatambua pamoja na mambo mengine mfumo wa kutambua viashiria vinavyoweza kuleta mapigano na kutishia amani na usalama duniani, ukiukwaji wa haki za binadamu na uwajibishaji wale wanaokiuka haki za binadamu.

Awali Katibu Mkuu Ban Ki-Moon alitumia hotuba yake kutoa shukrani kwa Kamishna wa haki za binadamu Navi Pillay aliyetuhutubia baraza hilo kwa mara ya mwisho kwani wadhifa wake unafikia ukomo mwishoni mwa mwezi huu, na ndipo akaangazia amani na usalama.

(Sauti ya Ban)

"Lakini  pindi kunapokuwepo na uelewano mdogo, pindi hatua zetu zinapochelewa na hatimaye tunachukua hatua dhidi ya jambo dogo sana, matokeo yake yanaweza kupimwa kwa kuwepo kwa idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha, machungu makubwa ya binadamu, na kupotea kabisa kwa imani ya watu kwa baraza hili na umoja wetu. Hakuna changamoto kubwa mbele yetu zaidi ya kuimarisha uwezo wetu wa kuafikiana mapema.”

Bi. Pillay akasema utambuzi mapema wa mizozo ni jambo muhimu kwani unaepusha madhara makubwa akitolea mfano mfumo unaotumiwa na Colombia.

(Sauti ya Pillay)

"Tuliwezesha kutambuliwa kwa  kiasi cha juu kwa mamlaka  za kijadi, mazungumzo yalichangia katika kutatua mizozo ya kijamii. Mfano wa kuigwa ni mfumo wa Colombia wa kuchunguza na kubaini mapema vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu"