Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola: Jukumu la UM ni kusaidia jamii kwa ujumla, unyanyapaa haufai

UN Photo/Mark Garten)
Dkt. David Nabarro, Mratibu wa UM kuhusu ugonjwa wa Ebola. (Picha:

Ebola: Jukumu la UM ni kusaidia jamii kwa ujumla, unyanyapaa haufai

Wiki moja baada ya kuteuliwa kuwa Mratibu Mwandamizi wa Umoja wa Mataifa kuhusu ugonjwa wa Ebola, Dkt. David Navarro amesema kesho anakwenda Afrika Magharibi ili abaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Umoja huo kusaidi raia, jamii na serikali zilizoathirika kwa ugonjwa huo.  Ataanzia Dakar, Senegal, halafu atakwenda Liberia, Sierra Leone, Guinea na hatimaye Nigeria.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York siku ya Jumanne, amesema jukumu la msingi la Umoja wa Mataifa ni kusaidia raia na jamii zao, na kuimarisha nguvu za serikali katika kupambana na Ebola hivyo jambo la msingi ni kuimarisha sekta ya afya katika shughuli zake za kuhudumia wagonjwa na kudhibiti maambukizi.

Hata hivyo ameongeza, Ebola inaweza kuathiri mfumo mzima wa jamii:

“ Inaathiri masuala ya kijamii na kiuchumi, inaathiri utawala, inaweza kuwa na matokeo ya kibinadamu na ya kisiasa, inaweza hata kuwa na athari katika masuala ya usalama. Kwa hiyo, tunahitaji jibu la ujumla kwa kutumia mbinu zote na uwezo wote uliopo kwenye mfumo wetu wa Umoja wa Mataifa”

Halikadhalika Dokta Nabarro amesema jukumu la Umoja wa Mataifa pia ni kuhakikisha maambukizi hayasambai dunia kote.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, amekaribisha uamuzi wa shirika la afya duniani WHO wa kutafuta njia ya kuwapatia wagonjwa dawa mpya la majaribio ili kutibu Ebola.

Aidha, ameelezea kusikitishwa na unyanyapaa unaokumba wagonjwa wa Ebola waliopona na wanaotaka kurudi makwao, akisema ni muhimu waandishi wa habari washirikiane katika kuelimisha jamii ili kupambana na unyanyapaa.

Awali siku hii, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari kwamba idadi ya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola imefikia 1229.