Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yalaani urushaji risasi karibu na kambi ya wakimbizi Bentiu

UN Photo/Martine Perret
Kituo cha UNMISS.

UNMISS yalaani urushaji risasi karibu na kambi ya wakimbizi Bentiu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini, UNMISS umelaani tukio la Jumatatu usiku la ufyatuaji risasi angani uliofanyika karibu an kambi yake huko Bentiu, jimbo la Unity, tukio lililodumu kwa nusu saa.

Taarifa ya UNMISS inasema chanzo cha ufyatulianaji huo wa risasi hewani ni wanajeshi wa kikosi cha serikali SPLA walioko karibu na uwanja wa ndege wa  Rubkona ambao walikuwa wakisherehekea siku ya wazee waliopigana vita.

UNMISS inasema katika tukio hilo mtoto mmoja katika kambi ya kulinda raia alijeruhiwa, halikadhalikia UNMISS iliweza kupata risasi tisa zilizopenya mahala pa kulala na kwenye eneo linalotumika kama ofisi.

Ujumbe huo umesema unahofia mno tukio hilo ambapo raia walijeruhiwa na ingeweza kusababisha madhara makubwa kwa raia na wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa.

Kwa mantiki hiyo UNMISS imeisihi SPLA kutotumia risasi wakati wa sherehe zao karibu na eneo la ulinzi wa raia.