Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia yaongoza barani Afrika kwa kuhifadhi idadi kubwa ya wakimbizi

Wakimbizi waSudan Kusini wanoishi katika makazi ya muda wakisubiri mahema kutoka UNHCR.Ethipoia inawahifadhi zaidi ya wakimbizi 600,000.Picha© UNHCR/P.Wiggers

Ethiopia yaongoza barani Afrika kwa kuhifadhi idadi kubwa ya wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema hivi sasa Ethiopia inaongoza barani Afrika kwa kuhifadhi idadi kubwa ya wakimbizi, nafasi ambayo awali ilikuwa inashikiliwa na Kenya.

Kwa sasa Ethiopia inahifadhi wakimbizi karibu 630,000  ikiwa ni takwimu za hadi mwezi uliopita ilhali Kenya inahifadhi zaidi ya wakimbizi 575,000 waliosajiliwa na wasaka hifadhi.

Mizozo nchini Sudan Kusini imechochea ongezeko la wakimbizi Ethiopia, wakiwemo pia wasomali na waeritrea.

Kwa sasa UNHCR imesema inatoa misaada ya hifadhi kwenye kambi 23 na vituo vitano vya muda nchini Ethiopia vinavyohudumia wakimbizi kama anavyosema Adrian Edwards, msemaji wa shirika hilo Geneva.

(Sauti ya Adrian)

 “Kambi tatu kati ya hizo 23 ni mpya pamoja na vituo hivyo vya muda na vilifunguliwa mwanzoni mwa mwaka huu kufuatia kumiminika kwa wakimbizi wanaotoka Sudan Kusini. Kambi hizo tatu zimejaa na UNHCR inatengeneza nyingine mbili. Wakati wakimbizi wanasubiri kuhamishiwa kambi mpya, zaidi ya wakimbizi 18,000 wamehifadhiwa kwenye vituo hivyo vitatu vya muda vilivyoko eneo la magharibi la Gambella. Hata hivyo wiki za karibuni mvua kubwa zimesababisha kufurika maeneo haya kwani yako ukanda wa chini na kambi ya Leitchuor ambako hali ni mbaya. Takribani wakimbizi 10,000 zaidi ya moja ya tano ya wakimbizi 47,600 kwenye kambi hiyo ya Leitchuor wamekumbwa na mafuriko. Mahema mengi na makazi yamefunikwa kwa maji halikadhalika vyoo vimebomoka. Hii inatia wasiwasi sana suala la afya na inatishia mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti mkurupuko wa magonjwa yanayoenezwa na maji machafu. Wakimbizi wamejenga mahema kwenye maeneo ya juu.”

 Hadi kufikia katikati ya mwezi huu, raia Milioni Moja nukta Nane wa Sudan Kusini wamelazimika kukimbia makazi yao ambapo kati yao Milioni 1.3 ni wakimbizi wa ndani na zaidi ya 575,000 wamekimbilia nchi jirani.