Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yazindua operesheni kabambe ya kufikisha misaada kaskazini mwa Iraq

Watoa huduma wakati wa kuwasilisha misaada kwa watu waliolazimika kukimbia makwao.Picha© UNHCR/E.Colt

UNHCR yazindua operesheni kabambe ya kufikisha misaada kaskazini mwa Iraq

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR, linazindua operesheni kabambe ya kuwafikishia misaada takriban watu nusu milioni ambao wamelazimika kuhama makwao kaskazini mwa Iraq.

Operesheni hiyo ya kusafirisha misaada kwa njia ya angani, barabara na bahari, itaanza hapo kesho Jumatano kwa usafirishaji wa shehena za misaada kwa ndege kutoka Aqaba, Jordan kwenda Erbil kwa kipindi cha siku nne, ukifuatiwa na misafara ya barabarani kutoka Uturuki na Jordan, na shehena za baharini kutoka Dubai.

Watu waliolazimika kuhama makwao, hususan kutoka jamii za walio wachache, wametafuta hifadhi katika kata ya Dohuk, jimbo la Kurdistan, wakikimbia ukatili ulioanza kutekelezwa na kundi la Waislamu wenye msimamomkali, ISIL, kwenye mji wa Sinjar na maeneo jirani.

Adrian Edwards, msemaji wa UNHCR amesema matatizo ya kibinadamu Iraq sasa hivi ni makubwa, huku wengi wa watu waliolazimika kuhama wakiwa wanaishi katika mazingira duni katika shule, misikiti, makanisa na majengo ambayo hayajakamilika.

“La kuangaziwa na kuboresha hali ya maisha kwa wakimbizi katika eneo hilo, hususan watu wasio na makazi au nyumba. Hali ni mbaya mno kwa wale wasio na makazi, wanaohangaika kupata chakula kulisha familia zao, na wale wasio na huduma za kimsingi za afya. Wengi wanakabiliana na janga ambalo wameshuhudia katika wiki chache zilizopita, kama kukimbia makwao bila chochote na kupoteza wapendwa wao. Usaidizi unahitajika kwa dharura na tunajaribu kuutoa.”

Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa ulitangaza daraja ya juu kabisa ya dharura kwa hali nchini Iraq, ili kuwezesha uchagizaji wa misaada zaidi ili kukidhi mahitaji yanayozidi kuongezeka ya watu wapatao milioni 1.2 waliolazimika kuhama makwao tangu mwanzoni mwa mwaka huu.