Gaza nzima inahitajika kujengwa upya; Baraza la Usalama laelezwa

18 Agosti 2014

Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mashariki ya Kati, Robert Serry, aliyeshiriki kwenye mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestine, huko Misri, amezungumza mbele ya Baraza la Usalama na kusema kuwa mazungumzo hayo ni muhimu sana ili kusitisha mkwamo wa vitendo vya ghasia na kulipiza visasi.

Ameziomba pande zote zifikie makubaliano yatakayoangazia mizizi ya mgogoro huo, yakiwemo kuzungirwa kwa Gaza, na ugaidi unaotishia Israel.

Serry amelieleza baraza hilo kwamba kiwango cha uharibifu wa Gaza ni cha juu sana, na hivi ukarabati unahitajika popote kwa ujumla, kwa kushirikisha sekta binafsi na serikali.

Amesisitiza umuhimu kwa Gaza kuruhusiwa kuingiza vifaa vya ujenzi kwa ukarabati huo, akisema Umoja wa Mataifa unaweza kusaidia kuthibitisha matumizi hayo yasiwe kwa ajili ya kujenga tena njia za chini ya ardhi zilizopigwa na Israel, akisemea Gaza inahitaji nyumba, shule na hospitali, si roketi, mapigano wala njia za chini ya ardhi.

Hatimaye amelikumbusha baraza la usalama kwamba majengo ya Umoja wa Mataifa yalipigwa na makombora, raia 38 wakifariki dunia katika mashambulizi hayo wakiwemo wafanyakazi 11 wa UNRWA, na kwamba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameomba uchunguzi ufanyike juu ya vitendo hivyo.