Kuzingirwa kwa Gaza ni adhabu inayopaswa kuondolewa

18 Agosti 2014

Wakati baraza la usalama likikutana leo kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, Pierre Krahenbuhl, ambaye ni mkurungenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA, ameomba Israel isitishe kitendo chake cha kuzingira Ukanda wa Gaza kilichodumu kwa miaka saba, akisema ni adhabu kwa wakazi wote wa Gaza.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Gaza, Krahebuhl amesema bado raia zaidi ya milioni 1.1 wanategemea misaada ya UNRWA:

“ Ni dalili inayoonyesha jinsi gani raia wameathirika sana na mapigano hayo, lakini pia na kuzingirwa, na vile vile na mapigano mengine yaliyotangulia”

Krahenbuhl amesema, UNRWA na familia nzima ya Umoja wa Mataifa itaendelea kusaidia raia huko Gaza, iwe kupitia misaada ya dharura, misaada ya kisaikolojia au kujenga upya eneo lao:

“ Tunahitaji kutuma ujumbe wa matumaini kwa wakazi wa Gaza, tunahitaji uhuru kwa watu, uhuru wa kutembea, kufanya biashara na kushiriki shughuli zote za maisha ya kawaida. Hayo ndiyo matarajio ya msingi ya kila mtu duniani”

Katika ziara yake kwenye ukanda wa Gaza, ametembelea shule zote za UNRWA zilizopigwa na makombora ya Israel ambapo watu kadhaa wamepoteza maisha, wakiwemo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, akisisitiza kwamba vitendo hivyo avikubaliki na UNRWa itaendelea kuomba uchunguzi ufanyike juu ya uhalifu huo.