Mashirika Sita ikiwemo WHO yazindua kikosi kazi kudhibiti Ebola

18 Agosti 2014

Kikosi kazi cha masuala ya safari na usafirishaji kinachoundwa na mashirika Sita likiwemo lile la afya duniani WHO, kimeanza kazi ili kudhibiti uwezekano wa kirusi cha Ebola kusambazwa wakati wa safari za anga.

WHO na mashirika hayo mengine ya kimataifa likiwemo lile la mamlaka ya anga, ICAO, utalii UNWTO, baraza la viwanja vya ndege ACI, usafirishaji wa anga duniani, IATA na baraza la utalii na usafirishaji WTTC wamezindua utendaji wa kikosi kazi hicho Jumatatu.

Kikosi hicho kitafuatilia hali ya Ebola ilivyo na kusambaza taarifa wakati muafaka kwa sekta zote za usafirishaji wa anga na utalii pamoja na kwa wasafiri wenyewe.

WHO imesema uwezekano wa msafiri wa anga kuambukizwa kirusi hicho bado ni mdogo, lakini wasafiri wanapaswa kila wakati kuzingatia usafri ikiwemo kuosha mikono yao.

WHO imetaka nchi ambazo bado hazijakumbwa na Ebola kuimarisha uwezo wao wa kuchunguza na kudhibiti visa vipya huku zikichukua hatau zitakazoepusha mazingira yanayoweza kukwamisha biashara na safari za kimataifa.

Hadi sasa Ebola imesababisha vifo vya watu zaidi ya 1069 tangu uibuke huko Guinea, Liberia, Sierra Leona mwezi Machi mwaka huu na sasa umeshaingia Nigeria.